BIMA: HUDUMA MPYA ITOLEWAYO NA BENKI NYINGI NCHINI

Na Kamugisha Rwechungura, Mwanachama wa TIOB

Published: 23/May/2018, Mtanzania Newspaper

 

Hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya kibenki nchini. Mabadiliko haya yamechochewa na maendeleo ya teknolojia pamoja na juhudi za serikali inazozifanya katika kuweka na kutekeleza sera mbalimbali zenye lengo la kuendeleza sekta hiyo. Mabadiliko ambayo ni dhahiri ni pamoja na kukua kwa kiasi kikubwa kwa sekta ya kibenki ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini. Kutokana na kutungwa kwa sheria mpya hasa  ile Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha (Banking and Financial Institutions Act) ya mwaka 1991 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006; sekta ya kibenki nchini imebadilika sana. Sheria hii iliruhusu uanzishwaji wa benki binafsi pamoja na kuruhusu benki za kigeni kuingia na kufanya biashara hapa nchini. Uingiaji wa benki za kigeni na uanzishwaji wa benki binafsi nchini umetia chachu ya maendeleo ya sekta ya kibenki nchini. Benki zimeanza kutumia njia mpya za usambazaji wa huduma zao kama kutumia simu, wakala na intaneti ili kuweza kuwafikia wateja wao kwa urahisi. Kati ya huduma mpya itolewayo na benki nyingi nchini ambayo watanzania wengi wana uelewa mdogo ni huduma ya bima (bancassurance).    

 

Neno “bancassurance” hutumika kueleza kitendo cha huduma za bima kutolewa na benki. Watu wengi hawajui kuwa kwa sasa benki nyingi nchini zinatoa huduma za bima. Kwa hiyo wanapokuwa wanahitaji huduma za bima kwa ajili ya mali zao kama magari na nyumba, wanakuwa hawafikirii kwenda kukata bima benki ila uenda kwenye makampuni ya bima waliyoyazoea tokea siku za nyuma. Watu wameendelea kuamini kuwa kazi pekee za  benki ni utoaji wa huduma za mikopo na amana. Benki zinazotoa huduma za bima nchini zinatoa huduma hii zenyewe kwa kujisimamia au kama wakala wa makampuni ya bima. Benki zinazotoa huduma hii hupata kipato cha ziada juu ya kile kilichozoeleka cha kwenye riba ya mikopo. Hivyo basi kama biashara ya utoaji wa huduma hii itaonekana yenye faida, tutegemee benki nyingi zaidi kuanza kutoa huduma hii.

 

Ripoti za Finscope za mwaka 2006, 2009, 2013 na mwaka 2017 zinaonyesha kuwa watanzania wengi hawatumii huduma za bima. Bima iliyoonekana kuwa na watumiaji wengi ni bima ya afya ikifuatiwa na bima ya magari. Bima ya majengo, bima ya ajali na bima ya maisha zimeonekana kuwa na wateja wachache sana. Bima ya Afya imeonekana kutumika na watanzania wengi huenda kwa kuwa ni lazima kwa kila mtumishi wa umma na baadhi ya makampuni binafsi kuwa na bima ya afya. Bima ya magari pia imeonekana kuwa na watumiaji wengi kwa kuwa ni kosa la kisheria gari kutembea barabarani lisipokuwa na bima. Kwa zile bima ambazo ni za hiari, watu wachache sana wamekuwa wakijitokeza kuzitumia. Hii inaonyesha kwamba, jamii ya kitanzania haitumii huduma za bima kwa kuwa haijajua umuhimu wake. Bima ina faida sana kwa mtu binafsi, mfanyabiashara na kampuni kwa ujumla.   

 

Mtu hukatia bima kitu chake cha thamani kama gari au jengo ili aweze kurudishiwa mali yake hiyo pindi litakapotokea tukio la kuharibu mali yake hiyo. Kwa hiyo lengo la bima ni kumrudisha mkataji wa bima katika hali aliyokuwa nayo kabla mali yake aliyoikatia bima haijaharibiwa. Kwa mfano, kama mteja wa bima alikuwa anamiliki gari halafu akapata ajali na gari lake likaharibika vibaya, basi kampuni ya bima itampatia gari jingine lenye thamani sawa na gari alilokuwa nalo kabla ya kupata ajali kwa kufuata masharti na vigezo vya bima hiyo.  Kwa maana nyingine ni kuwa mkataji wa bima anakuwa hajapata hasara kwani bima itamrudishia mali yake. Hii ndiyo faida kubwa ya bima maana inaondoa uwezekano wa mtu kupata hasara pale mali yake ya thamani inapokuwa imeharibika. Fikiria pale nyumba ya mtu inapoungua, kama anakuwa hajakata bima ya moto, nyumba yake inakuwa imepotea. Lakini anapokuwa na bima, kampuni ya bima itamjengea nyumba yenye thamani sawa na bima ya nyumba iliyoungua, hivyo atakuwa hajapata hasara. Kwa hiyo ni muhimu sana kwa kila mtu kukatia bima vitu vyake vya thamani ili kuepukana na hasara anayoweza kuipata pindi ajali ikitokea na kuharibu mali yake.

 

Kampuni ya bima humlipa mteja wake aliyepata hasara ya kuharibikiwa na mali yake kwa pesa taslimu yenye thamani sawa na mali iliyoharibika au kwa kumpatia mali mpya yenye thamani sawa na mali iliyoharibika au kwa kumtengenezea mali yake iliyoharibika. Pamoja na kuwa ni kawaida kwa kampuni ya bima kumlipa mteja mali yake aliyoikatia bima pindi inapoharibika, kuna mambo muhimu mteja wa kampuni ya bima anatakiwa ayajue.

 

Moja, mkataji wa bima ni lazima atoe taarifa zote muhimu juu ya mali yake anayoikatia bima kwa kampuni ya bima au benki husika. Kama kutatokea hasara kwenye mali iliyokatiwa bima, na ikaja kujulikana kuwa kuna taarifa muhimu mkataji wa bima hakuzitoa kwa makusudi wakati anakata bima, huenda madai yake yakakataliwa. Kwa mfano, mtu anaenda kukatia nyumba yake bima dhidi ya moto na mafuriko, wakati anakata bima hiyo akaificha kampuni ya bima kuwa nyumba yake ina matatizo kwenye mfumo wa umeme. Ikitokea nyumba hiyo ikaharibiwa na moto ambao umesababishwa na umeme na kampuni ya bima ikaja kujua kuwa mteja wao alijua kuwa nyumba yake ina historia ya tatizo la umeme lakini hakuweka wazi; kampuni ya bima inaweza isimlipe mtu huyo au kumlipa kiasi kidogo cha hasara. Mteja anatakiwa kusema ukweli mtupu na kutoa taarifa zote za muhimu za mali yake anayoikatia bima ili kampuni ya bima iweze kumtoza kiasi cha pesa kama ada ya bima kinachostahili kutokana na hali ya mali yenyewe.

 

Mbili, mkataji wa bima anapokuwa amepata hasara kwa kuharibikiwa na kitu chake cha thamani alichokikatia bima; kampuni ya bima itamtengenezea mali yake au italipa fidia.  Baada ya kumlipa mteja wake huyo, kampuni inaweza kumdai mtu aliyesababisha hasara hiyo kwa kutumia jina la mteja. Kwa mfano, Salum kakata bima dhidi ya moto na mafuriko kwa nyumba yake isiyo na hitilafu yoyote, lakini ikaungua moto kwa hitilafu ya mfumo wa kampuni ya umeme husika, basi  Salum akienda kwenye kampuni ya bima atalipwa kulingana na masharti ya bima aliyokata na kampuni ya bima inaweza kushitaki kampuni ya umeme husika kwa kutumia jina la Salum. Kama kampuni hiyo ya umeme italipa fidia kwa ajali iliyoisababisha, fedha hizo zitachukuliwa na kampuni ya bima na wala si Salum kwa sababu lengo la bima si kumfaidisha mkata bima, bali ni kumrejesha katika hali yake ya mwanzo aliyokuwa nayo kabla hajapata ajali.

 

Tatu, kama mtu amekatia bima mali  yake (kwa mfano gari) katika kampuni za bima zaidi ya moja; inapotokea amepata hasara ya kuharibikiwa na mali yake hiyo, kampuni zote za bima zitachangia na kumrudishia mali yake hiyo. Kila kampuni ya bima inayohusika katika ulipaji wa mali hiyo italipa kulingana na kiasi ambacho mteja alikuwa anailipa kampuni hiyo dhidi ya mali husika. Ikumbukwe kwamba lengo la bima si kumnufaisha mteja bali kumrudisha katika hali yake aliyokuwa nayo mwanzo kabla hajapata tatizo. Hivyo basi, kampuni zote za bima alikokata bima juu ya mali yake iliyoharibiwa zitachanga na kumrudishia mali yake.

 

Ni dhahiri kwamba ukatiaji bima kwa vitu vya thamani una faida kubwa sana, hivyo  ni muhimu kwa  wantanzania kutumia huduma hii. Benki zimetusogezea huduma hii karibu na hivyo inapatikana kwa urahisi zaidi.  Wananchi kwa ujumla wanahamasishwa  kutumia benki pamoja na kampuni nyingine za bima ama wakala wao kupata huduma hii ili kuepukana na hasara zisizotegemewa pindi mali zinapoharibika kwa ajali. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa  baadhi ya watumiaji wa huduma za bima kama kuchelewa kulipwa na makampuni ya bima husika pale mali walizozikatia bima zinapoharibika kwa ajali. Pia wengine wamesema kuwa kuna mlolongo mrefu sana unaotakiwa kufuatwa ili mtu aweze kulipwa. Wakati tunaendelea kuhamasisha umma wa watanzania wengi kutumia huduma za bima; mamlaka husika inayosimamia maswala ya bima nchini (Tanzania Insurance Regulatory Authority) inaombwa kuangalia  changamoto hizi ambazo zinaonekana kuwa kero kwa watumiaji wa huduma za bima nchini.