UAMINIFU WA MTEJA NI FURAHA KUBWA KWA BENKI

 

Na Na Jackson Rutahinzibwa, Mwanachama wa TIOB
Published: 15/May/2018, Mtanzania Newspaper

 

Taasisi za fedha ni nyenzo imara katika kuendeleza na kuchochea mafanikio ya kiuchumi ya kundi kubwa la watu. Nia ya uwepo wa mabenki duniani ni kuwezesha shughuli za uchumi kufanyika kwa uhakika kwa kuwa mitaji ndiko inakopatikana. Mitaji hiyo hupatikana baada ya mabenki kuchukua amana kutoka kwa umma na kukopesha. Kwa kawaida benki husimama katikati ya watu wenye fedha ya ziada na kutumia fedha hiyo kuwekeza. Wenye fedha za ziada ni wateja wa benki na wenye uhitaji (wakopaji) nao ni wateja wa benki. Hii inatofautisha benki na biashara nyingine. Wafanyabiashara wa biashara nyingine wanaowauzia bidhaa/huduma ndio wateja na wanakonunua bidhaa hawawaiti wateja. Ili benki iweze kufanya biashara yenye faida wenye vigezo maalumu kwa pande zote yaani wanaoweka amana na wanaotoa. Kutokana na sababu hiyo, taasisi hizo za fedha zikiongozwa na mabenki huweka mikakati ya kuanzisha, kuendeleza na kusimamia mikakati yao kwa ustawi wa taasisi, wateja na uchumi kwa ujumla.

 

Mojawapo ya mikakati inayosisitizwa na mabenki ni upatikanaji na uendelezwaji wa wateja kwa ajili kuwa na uhakika wa faida na kuendesha shughuli zao. Mteja wa benki ni mtu anayehusika moja kwa moja katika shughuli za kibenki na hutegemewa sana na taasisi husika kwa sababu ndiye nyenzo ya mafanikio ya pande zote mbili.

 

Kila wakati mabenki yamekuwa yakiweka mikakati ya kutafuta wateja. Ukisoma mipango mikakati ya mabenki utakuta yameweka malengo ya kupata wateja. Aidha baadhi ya mabenki yameweka idara maalum kwa ajili ya kuratibu mikakati ya kutafuta na kuongeza wateja. Pia mabenki mengine huajiri wafanyakazi maalum wanaozunguka kuwashawishi watu katika maeneo mbalimbali kufungua akaunti kwenye benki hizo au kukopa. Wakati mwingine mabenki huweka vibanda sehemu mbalimbali vya kusajilia wateja (kufungua akaunti) pamoja na kuelezea huduma zitolewazo na banki husika.

 

Je, benki zina uhaba wa wateja? Ukiangalia utakuta taasisi nyingine zitoazo huduma zinazokaribiana na zile za benki zina wateja japokuwa nyingine ni ghali lakini wateja bado wanaziendea kutafuta huduma. Hapo tunakuja kugundua ya kwamba tatizo sio wateja bali ni aina na ubora wa mteja anayetakiwa na benki.

 

Benki huhitaji wateja ambao itaweka mahusiano nao kwa ajili ya biashara ya sasa na ya siku za usoni. Kabla mtu hajawa mteja wa benki lazima apitie kwenye chujio ili kuweza kubaini kama anaweza kuwa na vigezo. Anapokidhi vigezo hivi ndipo benki inaweka uhusiano naye.

 

Ili mteja aweze kukubalika na benki lazima awe mwaminifu. Biashara ya benki inahitaji uaminifu wa hali ya juu. Kuwepo watu wengi ambao sio waaminfu ndiko kunakochangia kwa kiasi kikubwa mabenki kuweka masharti magumu ili kuweza kupata huduma. Watu wengi pia wamekataliwa kupewa huduma na baadhi ya mabenki kwa sababu walikosa uaminfu kwenye benki nyingine baada ya kupata taarifa zao za mikopo kutoka taasisi zinazokusanya taarifa kutoka kwa wateja “Credit Reference Bureau”.

 

Wakati mwingine kumekuwepo na nadharia ya kwamba mtu wa kigeni anakuja na begi la nguo lakini baada ya muda mfupi anajiendeleza na kuwa bilionea kwa fedha na rasilimali za Tanzania. Hii inatokana na uaminifu ambao unamjengea sifa njema kwa sababu ya nidhamu ya fedha na kuzitambua fursa zilizopo nchini. Watanzania wakijifunza uaminifu utasaidia sana kupata mitaji kwa njia nyepesi sio tu kutoka kwenye mabenki lakini pia hata kwenye taasisi nyingine za kukopesha. Aidha wakiwa waaminifu kuna fedha nyingi za serikali zinazotolewa kwenye vikundi na nyingine kutoka kwa mashirika wahisani ya kimataifa. Hizi fedha zote zingeweza kuleta maendeleo makubwa ikiwa ni pamoja na kusababisha ajira pamoja na kukuza uchumi.

 

Tabia ya mteja humpa zaidi uwezekano wa kupata huduma awapo benki. Mienendo ya mteja jinsi anavyoitumia benki inaweza kumuongezea sifa zaidi. Kama mteja ana tabia ya kila anapopata pesa anaziweka amana benki na anazitoa wakati wa kuzitumia hii inasaidia sana huyo mteja kuaminika lakini pia kupata huduma nyingine kwa urahisi zaidi. Akiweka na kutoa mara kwa mara akaunti yake itaonesha mzunguko mkubwa ambao kimsingi mabenki hupenda sana kukopesha mteja wa namna hiyo.

 

Mteja anayechukua mkopo uitwao “overdraft” ambapo mteja huruhusiwa kutoa kiasi cha fedha kwenye akaunti yake hadi kikomo fulani huhitajika kuwa na uaminifu yakinifu. Mikopo hii kwa mteja ambaye anazingatia kuweka na kutoa pesa mara kwa mara humuwezesha kuonesha uwezo wa mteja huyo kufanya manunuzi na kuuza hivyo kuwa na uwezo wa kumaliza deni.

 

Aidha benki hupenda wateja ambao wanaweka mahusiano ya muda mrefu. Kuna baadhi ya wateja ambao wanakuwa na mahusiano ya karibu na benki. Wengine hufika hatua ya kufahamiana na wafanyakazi wa tawi la benki husika. Kutokana na mahusiano mazuri, wafanyakazi wa tawi la benki wanaweza kuzuia wizi ambao unaweza kufanyika kwenye akaunti ya mteja. Mfano mhalifu akigushi hundi wafanyakazi wa benki ambao hundi itapitishiwa kwao wanaweza kutilia mashaka uhalifu huo na hatimaye kuzuia wizi usitokee.

 

Kutokana na uhalisia ulioelezwa hapo juu, ni malengo ya mabenki kuhakikisha wanapata wateja wenye uhakika wa kushirikiana nao. Mtu anayeelewa biashara hawezi kubeza juhudi zinazowekwa na za taasisi za fedha kuendeleza biashara kati yake na mteja. Wateja wanahamishwa kufahamu fursa iliyojificha katika kutumia mabenki kwa ufasaha kwa sababu huwezesha upatikanaji wa mitaji na kuendeleza biashara kwa umakini mkubwa.

 

Ifahamike kwamba mabenki hupewa kibali na Benki Kuu za mataifa duniani ili kupokea amana za wateja ambazo huzitumia kuendeleza shughuli za kiuchumi, kubwa ikiwa ni kutoa mikopo kwa wateja. Hivyo ni usumbufu kwa mabenki pale mteja anaposhindwa kurejesha mkopo kwani fedha hizo ni miliki za wateja wake, kwa hiyo mabenki hujikuta katika hatari (risk) ya kushindwa kumpatia mteja fedha yake anapoihitaji.

 

Taasisi ya fedha yenye uhakika na mteja mwaminifu hufurahia na kutamani kumuendeleza kadiri iwezavyo. Tena wakati mwingine mabenki huwa tayari kuingia gharama ili mradi kuhakikisha mteja huyo anaendelea na kupanua shughuli yake ya kibiashara. Hiyo ndiyo siri ya uhusiano mzuri kati ya mteja na benki yake. Jamii yote inahimizwa kuzingatia uaminifu na kuchukua mikopo waliyo na uwezo wa kulipa, pia kujitahidi kutumia mikopo yao kwenye shughuli zilizolengwa ili shilingi iweze kuzaa nyingine na kulipa kwa wakati.