Akiba Haiozi

Na Simon Goodness Musiba

Published: 09/Jan/2018, Mtanzania Newspaper

 

Tukiwa tumeuanza mwaka 2018 kila kijana, mzazi, mlezi, na mtoto wana malengo yao ya kufanikisha ndani ya mwaka huu mpya baada ya tathmini ya utekelezaji wa malengo yao kwa mwaka 2017. Malengo haya yanatokana na uzoefu wa mwaka jana na mwangaza wa leo.

 

Malengo mengi tunayoweka yanahitaji fedha katika utekelezaji wake na hususani katika kujikwamua na janga la ukosefu wa ajira kwa vijana, kukuza biashara, na kufikia malengo mengine binafsi kama kumiliki nyumba, kununua gari na kukidhi ada ya masomo kwa elimu ya juu. Kumekuwa na suala zima la vijana kutokopesheka wanapotafuta mikopo kutoka taasisi za fedha hivyo kuwaathiri katika suala zima la uchumi wao binafsi na taifa kupoteza mapato mengi kwa kupoteza kodi kwa vijana hawa wachapakazi. Hali hii hutokana na kutokidhi masharti yaliyowekwa na taasisi hizi nchini kwa kutokuwa na dhamana zinazokubalika na benki na dhana ya kwamba vijana waliohitimu hawana uzoefu (fresh graduates).

 

Nini Chanzo?

Kiini cha tatizo tatizo hili kinatokana na vijana na watanzania kwa ujumla kutokuwa na asili ya kutumia huduma za kibenki tangu awali hivyo hata kushindwa kujiwekea akiba katika taasisi za kifedha. Uwekaji wa akiba humwezesha mteja kutambuliwa katika mfumo wa benki na mzunguko wake wa fedha, kitu ambacho ni muhimu sana wakati wa uchambuzi wa maombi ya mkopo.

 

Ni vigumu benki kumkopesha mteja anayeanza biashara (Start-up business loans) kutokana na nadharia zilizosheheni katika mipango ya biashara kuliko uhalisia wake na kukosa uzoefu katika uendeshaji wa biashara hiyo. Kutokana na kutokutumia huduma za kibenki mteja hukosa sifa kwa kutojiridhisha na mzunguko wake wa fedha na kuashiria mkopo kutolipika kwa urahisi.

 

Nini umuhimu wa akiba?

Kwanza, kujiwekea utamaduni wa kuweka akiba humsaidia mteja kupata fedha zake wakati anapohitaji, Pili, humwezesha kupata riba kutokana na uwekezaji wake katika taasisi hiyo ya fedha kuliko kukaa na pesa taslimu isiyozaa (non-interest earning asset).

 

Akiba (FDR- Fixed Deposit Receipts) hutumika kama dhamana ya mkopo kwa wale wasio kuwa na dhamana kama vile hati ya kiwanja au nyumba na kwa wale waliokosa wadhamini ili waweze kupata mkopo. Mkopo wenye dhamana ya aina hii huwa na riba ndogo kutokana na athari zake kuwa ndogo kuliko dhamana zote.

 

Kwa nini tuvunje vibubu?

Wengi wametumia vibubu kama njia ya kujiwekea akiba kwa kusema wanaepuka gharama za benki lakini imewawia vigumu sana kwa wengi wao kutokuwa na nidhamu ya fedha (financial discipline), pia ukosefu wa usalama wa fedha za vibubu kama vile kuibiwa na makazi kuharibiwa.

 

Sababu nyingine ya kuvunja vibubu na kuhamia kwenye taasisi za kifedha ni usalama wa fedha kwenye mabenki, kupata faida au riba kutokana na akiba inayowekwa, kupata huduma nyinginezo kama vile mikopo na kutambulika rasmi katika mfumo wa kibenki. Utambuzi huu huzisaidia benki pindi zinapofanya uchambuzi wa mkopo kwa mteja kufanya uchambuzi yakinifu na kutoa mkopo ulioko ndani ya uwezo wa mteja bila kuathiri ukuaji wake na urejeshaji wa mkopo huo.

 

Nini kifanyike?

Ili kujijengea mazingira ya kukopesheka, vijana wanapaswa kujenga utamaduni wa kutumia huduma za kibenki na kurasimisha shughuli zao na kuweka taarifa zao katika mfumo wa kibenki (database) na kuwezesha taasisi kutambua mzunguko wa fedha wakati wa uchambuzi wa maombi ya mkopo.

 

Wazazi na walezi ni wakati wa kuwawekea akiba watoto wao kwa kuwafungulia akaunti za akiba za watoto (Minor account). Hizi akaunti zitarithiwa na hawa watoto wanapofikisha umri wa miaka kumi na nane (18) hivyo kurahisisha na kuwaweka tayari kwa safari ya kujitegemea.

 

Vijana pia wana haja ya kujenga utamaduni wa kuungana katika vikundi na kutekeleza mipango yao pale wanapogundua kwamba hawawezi peke yao kwani kuna msemo usemao; “ukitaka kwenda haraka nenda peke yako na ukitaka kwenda mbali nenda na mwenzako”. Kuchagua mtu sahihi wa kuingia nae ubia ni jambo la msingi pia katika kufanikisha huu muungano maarufu kama partnership. Kila mmoja ana talanta yake hivyo hatuwezi kulingana na kila mmoja atatoa mchango wake kuliko angebaki peke yake, “Umoja ni nguvu na kidole kimoja hakivunji chawa”.

 

Nini mchango wa benki?

Kutokana na malalamiko ya wengi kukwepa makato ya miamala ya kibenki, ni jukumu la benki na taasisi za fedha kutoa elimu juu ya makato haya ambayo ni muhimu na yenye tija huku yakiendana na huduma wanayoipata (benefit) wateja kuliko hasara za kutokuweka akiba na kutumia vibubu. Sambamba na utoaji wa elimu ni dhahiri na yenye umuhimu mkubwa mabenki kufanya yafuatayo:

 

Moja, Taasisi zote za fedha zinatakiwa kuwa na usawa, uwazi na zenye uhakika na tegemezi katika uendeshaji wa shughuli za kibenki na kuhakikisha kila huduma zitolewazo na zinazoendelea kuzinduliwa gharama zake zisiwe na ubaguzi, kupendelea upande  au sekta yoyote na zisiwe za kujinufaisha kama taasisi kwa udanganyifu.

 

Pili, Haya yote yatafanikiwa endapo sheria za upangaji wa gharama za miamala zitafuatwa, ikiwa ni pamoja na kumtaarifu mteja kuhusu gharama na makato yote ya huduma aliyochagua, kuweka wazi taarifa za makato na gharama (Tariff guide/schedule) katika matawi yote ya benki pamoja na njia zingine za mawasiliano zinazotumiwa na benki na kumtaarifu mteja kuhusu ongezeko lolote la gharama anazopaswa kulipa anapohitaji huduma yoyote benki.

 

Niwatakie kila la kheri tunapojipanga kutekeleza haya yote kwa safari tulioianza mwaka huu 2018.

 

“Maskini huweka akiba, matajiri huwekeza”