Taasisi za Kifedha

Taarifa za kina kwa mwananchi juu ya uendeshaji wa Taasisi za Kifedha utachagiza kasi ya ukuaji wa Uchumi wetu

Na Jackson Rutahinzibwa (Mwanachama wa TIOB)

Published: 23/Jan/2018, Mtanzania Newspaper

 

Taarifa za kutosha kwa wananchi juu ya uendeshaji wa Taasisi za fedha ni jambo muhimu linaloweza kuisaidia jamii husika kujikomboa kiuchumi toka hatua moja kwenda hatua ya pili. Elimu juu ya huduma za kifedha maana yake ni kuwa na ufahamu wa huduma za kifedha zilizopo na kuweza kupambanua ni huduma gani inafaa kutumia kulingana na mahitaji yaliyopo.

 

Elimu hii inahusika na upatikanaji wa taasisi za kutoa mkopo unaohitajika, njia bora ya utunzaji wa mitaji na faida, njia bora za usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kadhalika. Watanzania wengi wamekuwa mbali na ufahamu wa huduma za kifedha na wakati mwingine hulazimika kuzilipia kwa gharama kubwa kuweza kizifikia. Hii ni kwa sababu ya kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya fedha unaoendana na kubaini fursa zilizopo. Aidha katika sekta ya fedha Tanzania, kuna baadhi ya huduma zinazopatikana lakini hazijaweza kuwa katika ufahamu wa wananchi kutokana na Elimu duni ya mambo ya kifedha (Financial Education).

 

Sekta ya huduma za kifedha ni kiungo muhimu kinachowezesha mfumo wa uchumi na fedha kufanya kazi vizuri na endelevu. Sekta hii ni nyeti sana na kutokana na umuhimu wake, serikali zote duniani huipa kipaumbele na kuisimamia kwa weledi wa hali ya juu. Ukuaji wa sekta hii unategemea sana wingi wa washiriki. Hapa Tanzania kuna taasisi za aina mbali mbali za kifedha ambazo zinahusika moja kwa moja katika kuhuisha mfumo huu kufanya kazi. Taasisi hizo ni pamoja na mabenki, taasisi za kutoa mikopo zisizokuwa mabenki, taasisi za bima, mifuko ya mafao kwa wastaafu, soko la hisa na uwekezaji kupitia vipande (Mfano UTT) na taasisi zinazotoa huduma za kipekee (Specialized Finance) kama vile benki za maendeleo, kampuni za karadha, kampuni za mikopo ya nyumba, benki zinazofuata taratibu za sharia ya Kiislamu pamoja na taasisi zinginezo zinazotoa uduma za kifedha. Uushiriki wa wananchi  kwenye taasisi hizi kutachagiza uwekezaji nchini kuongezeka ikiwemo sekta ya viwanda ambayo inatazamiwa kuchangia maendeleo ya Taifa hadi kufikia mwaka 2025.

 

Pamoja na changamoto hizo, ushiriki wa Watanzania kwenye huduma za fedha umekuwa ukiongezeka siku hadi siku. Ripoti ya Finscope ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa asilimia 65 ya Watanzania wenye umri wa watu wazima wanafikiwa na huduma rasmi za kifedha. Aidha ripoti hiyo inonesha zaidi kuwa asilimia 86 ya familia (households) nchini Tanzania zinaruhusu watu kuwa na simu za kiganjani. Umiliki wa simu huwezesha watu kuwa na fursa ya kufanya miamala kupitia simu zao. Kuongezeka kwa ushiriki wa watu katika mfumo wa fedha umechagizwa sana na teknoloji inayorahisisha kufanyika kwa miamala ya kifedha na kuwezesha huduma zifike maeneo mengi ikiwemo vijijini. Teknolojia ni mguu mmoja unaowezesha huduma jumuishi za kifedha (Financial Inclusion). Mguu wa pili ni watu kuwa na uelewa wa kutosha juu ya huduma za kifedha zilizopo. Mathalani watu wengi hutumia simu kufanya miamala ya kifedha hasa ya kutoa na kutuma pesa lakini sio wengi wanaoweza kulipa michango yao kwenye mifuko ya mafao ya uzeeni kwa kutumia mitandao hiyo ya simu.  

Taratibu na sheria za nchi huwahitaji wananchi kutoa kiasi fulani cha fedha kulipia bima kwa ajili ya kujilinda na kesho isiyotabirika na yenye uwezekano kuwa na gharama. Lakini ni wananchi wachache walio na ufahamu wa umuhimu wa huduma hii ambapo walio wengi huipata kwa kulazimishwa tu, ingawa ni kwa faida yao wenyewe Watu wangejua umuhimu wa kujilinda wasingekuwa wanalazimishwa na sheria ya usalama barabarani kulipia bima kwa wakati. Tena wengine hadi wakilipishwa faini mara kadhaa ndipo hulazimika kulipia bima zao.

 

Katika Mpango Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha 2018-2020 inalengwa kuwa hadi kufikia wakati huo angalau asilimia 75 ya Watanzania wenye umri mtu mzima wawe wanaweza kutumia mara kwa mara huduma rasmi za kifedha. Aidha mpango huo unalenga kufikia wakati huo asilimia 90 ya Watanzania wawe wamesogezewa upatikanaji wa huduma ya kifedha. Hii inatarajiwa kuendana sambamba na kusajili wakopaji kwenye taasisi za kukusanya na kutoa taarifa za kumbukumbu  za wakopaji (Credit Reference Bureaux), kusajili dhamana kwenye masijala ya dhamana na kuhakikisha asilimia 90 ya Watanzania wana vitambulisho vinavyokubalika (Kitambulisho cha Mpiga kura, kitambulisho cha uraia, paspoti ya kusafiria na leseni ya udereva).

 

Nchi zinazoendelea bado zinachangamoto kwa sababu kuna idadi kubwa ya watu wenye uelewa mdogo katika masuala ya fedha. Kwa upande wa Tanzania, serikali imeingia ubia kati ya umma na watu binafsi (Public-Private Initiative) na kuandaa mpango mkakati wa elimu fedha (National Financial Education Frame Work 2016-2020). Mpango mkakati huo umeahinisha walengwa na mbinu za kusambaza elimu ya huduma za fedha kwa wananchi.

 

Kwa kutokuwepo kwa elimu hiyo Watanzania walio wengi wamejikuta katika hali ngumu za maisha kutokana na kuingia kwenye mikataba kandamizi toka kwa baadhi ya tasisi za kifedha  na hivyo kuchangia kuongezeka kwa watu walio na mtanzamo hasi dhidi ya baadhi ya taasisi za fedha. Kwa mfano mwanandoa kutoa nyumba kama dhamana sharti mwenzi wake aweke sahihi ili taasisi ya fedha impatie mkopo. Hii imeshababisha wandandoa wengi kujikuta katika mtego wa kudanganywa na wenza kwa kuambiwa kuwa wao ni wadhamini tu wa mikopo na kusaini bila kuhoji.  Inapotokea mkopaji (mwanandoa) ameshindwa kulipa mkopo wake na hiyo nyumba kutakiwa kuuzwa, wanndoa wengi waliodanganywa wamejikuta katika wakati mgumu. Unakuta mwanandoa analalamika kuwa hakuridhia nyumba yao kukopewa fedha lakini fomu za mikopo zinaonesha aliweka saini yake. Hapa ndipo watu wengi hujikuta katika sintofahamu, hivyo elimu ya huduma za kifedha ni muhimu sana kwao. Katika jamii yetu watu wengi wamepata kadhia na madhara mengi kwa kukosa elimu ya huduma za fedha kama ifuatavyo:-

 

  • Wizi wa Mitandaoni

Elimu ya huduma za fedha inasaidia watu kutodhulumiwa na kupitia mitandaoni. Katka hili ipo mifano mingi sana ambapo watu wengi wamedhulumiwa. Watu hawa hupigiwa simu na kuambiwa wameshinda, hivyo watume pesa kiasi fulani ili kuidhinisha upokeaji wa kiasi kikubwa walichoshinda. Watu wengine wanapoteza simu zao ambako wamehifadhi nywila (neno la siri). Kwa kutumia namba hiyo mwizi anaweza kutoa pesa hiyo na kumsababishia hasara. Aidha kuna watu wanaandika nywila zao za kadi za benki kwenye madaftari yao. Hili humuwezesha mwanafamilia mwenye tabia ya wizi kuiona na kubeba kadi ya mmiliki ambayo humuwezesha kutoa pesa benki kwa urahisi sana. Wengine hunapigiwa simu wakiulizwa taarifa zao nyeti zinazowezesha wahahifu wa mmtandao kuwaibia pesa zao benki kwa urahisi.

 

  • Kughilibiwa kwa wateja na taasisi za kifedha

Baadhi ya taasisi hutoa taarifa zisizojitoshereza kwa ajili ya kupata wateja. Unakuta wanamwambia mteja akope kwa asilimia tano kwa mwezi. Kwa haraka haraka hii inaonekana kuwa nafuu kulinganisha na taasisi zinazotoza asilimia 20 kwa mwaka. Pamoja na kuwa hicho ni kiwango cha juu sana cha kukopa yaani asilimia 60 kwa mwaka, kutokana na kutokuwa ufahamu wa kutosha juu ya masuala ya kifedha wamteja wengi hufanya maamuzi yasiyokuwa makini (unsound decisions) na kufuata uelekeo usiyo sahihi.

 

  • Kujihusisha na taasisi hewa

Kumekuwa na kudhulumiwa kwa watu katika taasisi amabazo hazina vibali vya kufanya biashara. Mfano zimekuwepo taaisisi nyingi za upatu ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha kufanya watu wapate hasara badala ya kuwa suluhisho la mahitaji yao. Tumeshuudia taasisi nyingi zisizokuwepo zikijitokeza na kusababisha maumivu makubwa kwa wananchi.

  • Gharama za miamala

Utumiaji wa taasisi za kifedha huambatana na gharama kwa mteja. Kuna kanuni hutumiwa na taasisi za fedha kuweka makato kwa wateja. Nyingine hukata kulingana na kiwango cha muamala huku nyingine hupanga viwango kwa asilimia ya muamala. Mwananchi mwenye ufahamu juu ya viwango hivyo huweza kupanga ni njia ipi itamfaa kufanya muamala

  • Elimu ya Usimamizi wa Fedha

Kuna wananchi wengi wamejikuta katika sintofahamu baada ya kufanya matumizi tofauti na malengo ya mikopo yao. Mathalani mtu anapokopa shilingi Milioni 20 anaweza kuwa na mipango ya biashara, lakini anapomakwisha kupata hiyo pesa huishia kutumia kwa njia nyingine kabisa. Walio wengi hutumia kiasi fulani cha pesa ya mkopo kufurahia maisha na inayobaki ndiyo hufanya biashara. Huku ni kupindisha malengo ya mkopo na mwisho wa siku ulipaji wake hugeuka ndoto.

 

Wananchi wakiwa na elimu ya kutosha juu ya masuala ya kifedha watanufaika kama ifuatavyo:-

  • Uelewa wa masuala ya kifedha humuwezesha mtu kufanya maamuzi makini juu ya mapato na matumizi. Aidha, elimu ya huduma fedha humuwezesha mtu kuwa na mipango thabiti ya uwekezaji. Elimu ya kifedha hutumika kufanya ukokotoaji wa faida na hasara zinazopatikana kupitia huduma za fedha. kama vile marejesho ya mikopo ili kukwepa kudanganywa na maafisa wa taasisi za mikopo. Mathalani imeoneshwa katika utafiti wa Finscope 2017 kuwa asilimia 24 ya wafanyakazi wenye umri wa miaka 55 kwenda chini ndio pekee wenye mipango ya kustaafu. Aidha katika utafiti huo, asilimia 77 ya Watanzania  waliohojiwa ndio walionekana kutunza takwimu za matumizi yao huku asilimia 50 tu ndiyo waliokumbuka  kiasi walichotumia wiki moja iliyopita.
  • Mtu mwenye uelewa wa masuala ya kifedha huweza kubaini huduma mpya za fedha na kuzitumia kwa ufanisi. Dunia inabadilika kwa kasi kubwa hasa kwenye masual ya kifedha. Huduma mpya za kifedha zinashamiri duniani. Kwa sasa habari ya maarufu ya kimataifa ni sarafu ya kidijitari (cryptocurrency). Hii aina ya sarafu haijaweza kuruhusiwa kuendeshwa nchini Tanzania lakini mataifa mengi hasa nchi zilizoendelea zinakubalika kufanya miamala.
  • Elimu juu ya masula ya fedha unawezesha ushindani katika kutoa huduma za fedha kwa maana uwezekano wa kughilibu wateja unakuwa unapungua. Hivyo watoa huduma za kifedha lazima waboreshe na kutoa huduma bora zaidi kwa gharama nafuu.
  • Elimu juu ya masuala ya fedha unasaidia kulinda haki za wateja kwa ufasaha zaidi. Wateja wengi hawajui haki zao hivyo hushindwa kuzidai katika vyombo husika. Katika kutetea haki za mteja, serikali inaweza kutetea haki hizo kupitia vyombo vyake vya kisheria kwa urahisi. Kwanza mteja mwenye uelewa ataweza kutoa taarifa na pia anaweza kutoa ushahidi kwa ufasaha mbele ya vyombo vya sheria.
  • Natoa mwito kwa taasisi za serikali zenye jukumu la usimamizi wa taasisi hizi kuwa macho ili kubaini mianya inayotumiwa na wajanja wachache. Pia wadau wa masuala ya kifedha wanategemewa kuwapatia ufahamu wa kutosha wananchi juu ya ushiriki wao katika Uchumi Shirikishi. Kwa kuwa wajanja wengi hutumia mwanya wa uelewa mdog wa wananchi kuwaghilibu, ni wakati sasa wa kuwawezesha wananchi kuelewa ili kupunguza matatizo hayo. Wananchi pia tujitahidi kutafuta taarifa ili kupata ufahamu juu ya masuala ya kifedha ili kuwa huru katika nyanja hii.

 

Elimu juu ya taratibu na utoaji wa huduma za kifedha ni hatua muhimu kwa maendeleo ya jamii na ni nyenzo muhimu ya kuwezesha huduma ya fedha jumuishi. Aidha taasisi zinazotoa huduma ya kifedha hutegemea kupata mitaji kutokana na wateja wenyewe. Kwa mfano Mabenki yanakopesha amana na mashirika ya bima na mifuko ya mafao ya uzeeni huwekeza kutokana  na michango ya wanachama. Tumeshuhudia maendeleo mengi nchini kama vile Daraja la Nyerere Kigamboni jijini Dar es Salaam, Jengo la Machinga Complex pia la Dar es Salaam pamoja na viwanda mbalimbali vikianzishwa kutokana na uwekezaji wa mashirika ya hayo ya mafao ya uzeeni. Aidha makampuni mapya yenye mtaji mkubwa yangeweza kusajiliwa kupitia soko la hisa la Tanzania na kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama viwanda. Watanzania wangekuwa wanashiriki kikamilifu kuwekeza katika mifuko ya mafao ya uzeeni, mifuko hii ingekuwa na ukwasi wa kuwekeza zaidi kwenye maendeleo.

 

Mfumo mzuri  wa kifedha ni kiungo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa taifa lolote duniani. Mfumo wa kifedha ukiteteleka unaweza kusababisha madhara makubwa kwenye uzalishaji wa nchi husika. Mfumo wa kifedha ukiwa na washirika wengi unawezesha ukuaji wa uchumi kwa sababu fedha zinakuwa zinaelekezwa kutoka kwa watu au taasisi zisizokuwa na uhitaji wa fedha wakati huo na kupelekea watu au taasisi zenye uhitaji wa pesa kwa ajili ya kuzalisha. Sekta ya fedha inayoeleweka kwa wananchi ni kichocheo cha uhai wa uchumi na maendeleo ya taifa.